Kifungu cha ishirini na moja
Ponda: Habari yako Adili?
Adili: Nzuri sana Bw. Ponda. Labda zako, mimi nipo tu.
Ponda: Hata mimi ni salama salimini. Ninamshukuru Mungu kwa yote. Nimefurahi sana kukuona. Kwa siku nyingi, nimekuwa nikitaka tuonane.
Adili: Mbona! Yapo mageni au nini?
Ponda: Ah nawe! Tulia, ubaya wako ni wasiwasi mwingi. Wa nini wasiwasi. Iwapo huna haraka, tafadhali tuingie hapa tunywe soda ninapokueleza haja zangu.
Adili: Sawa Bw. Ponda. Ninaweza kutenga nusu saa hivi angalau utilize hamu yako.
Ponda: (Wanaingia hotelini na kuagiza soda). Kama ujuavyo, mficha maradhi kilio humfichua. Sitaficha ndwele na waganga ni tele. Aidha, akufaaye kwenye dhiki ndiye rafiki. Nimeonelea nije kwa msaada. Tatizo nililo nalo ni wewe tu uwezaye kunitatulia. Wewe ni rafiki yangu tangu utotoni. Kwa nini usinifae kwenye dhiki hii?
Adili: Mimi nitakusaidia iwapo nitaweza. Kama ujuavyo, mtu hujikuna ajipatapo na ukarimu usizidi uwezo. (Wote wawili wanacheka).
Ponda: Tatizo langu si kubwa kwako kwani wewe una satua na uwezo. Ninaweza sema ni kanda la usufi kwako ingawa kwangu ni zigo zito kama nanga. Kama ujuavyo, huwezi kuugua homa ukaenda kwa seremala utaenda kwa mganga na fungule mkononi ndiposa nimekuwa nikikutafuta.
Adili: Basi sema taabu yako. (Anaonyesha dalili za kukasirika)
Ponda: Bila shaka unamjua mwanamke yule wa kaka yangu. Kaka yule aliyeenda jongomeo mwaka jana?
Adili: Naam! Ninamfahamu sana Lulu. Hata juzi nilikutana naye cheteni. Maskini Lulu alijipata kizuka bado akiwa mchanga katika ndoa yake. Haidhuru, kalamu ya Mungu haikosi.
Ponda: Ni kweli kalamu yake Mola haikosi na vilevile mwiba wa kujidunga hauambiwi pole….
Adili: Mbona unasema hivyo lakini? (Anaonyesha mshangao)
Ponda: Iwapo huna habari, subiri nikueleze. Unajua penye urembo ndipo penye ulimbo? Lulu ndiye aliyesababisha kifo cha kaka yangu. Alienda kwa mramali mmoja eti apewe dawa ya kumfanya mumewe ampende zaidi. Dawa aliyopewa ikageuka kuwa sumu.
Adili: Kweli? Siamini!
Ponda: Amini kwani huo ndio ukweli. Sasa ninalotaka ni kukiwahi chuma kingali moto. Lulu aliachiwa shamba na kaka yangu. Ninasikia kuwa anadhamiria kuliuza shamba hilo. Sijapata uhakika wa habari hizo. Hata hivyo, lisemwalo lipo na kama halipo li njiani likija.
Adili: Endelea
Ponda: Ninataka unisaidie kuyabadilisha majina katika cheti miliki cha shamba lile. Jina lililoko katika cheti kile ni la marehemu Kaunda. Ninataka libadilishwe na kuwekwa langu.
Adili: Lakini hayo ni ya nini? Si mali ya nduguyo yanastahili kutunzwa na mkewe na watoto wake iwapo wana uwezo?
Ponda: Huo ni ukweli. Lakini sasa, mtunza wa mali ya hayati Kaunda ni nani? Ni huyu Lulu aliyemwangamiza? Mbona umwachie paka kitoweo! Lazima niingilie kati kuyanusuru mali ya ndugu yangu. Kumbuka damu ni damu si kitarasa. Sitaki kusubiri hadi maji yamwagike. La, nitaingilia kati ili wapwa wangu wasiteseke siku za usoni.
Adili: Hayo ya kukusaidia siwezi.
Ponda: Kwa nini usiweze bwana? Si wewe ni msajili katika idara husika? Kama ni pesa, za kulainisha koo unapoongea na wakubwa, usijali zipo. Hakuna cha bure siku hizi. Huu ni ulimwengu wa “Nipe nikupe.”
Adili: Lakini hicho ni kitendo cha ufisadi. Kumbuka serikali imejitolea kuiangamiza saratani hii ya ufisadi. Unataka nifungwe au nini? Usinidanganye kwa hela hizo chache sitaki kupoteza kazi yangu.
Ponda: Sio hivyo. Vita vya ufisadi ni handaa za mvua msimu wa kiangazi. Ni moto wa karatasi. Niko tayari kukupatia shillingi laki mbili na nusu pesa taslimu. Waonaje? Koma kujifanya mwadilifu. Kwani uadilifu huo utawapelekea watoto wako jioni wale kama kilalio? (Huku akitabasamu) Elewa pesa ni mvunja mlima. Amka bwana! Tembea na majira la sivyo …
Adili: Sizitaki pesa hizo. Hizo ni pesa chafu. Jitajirishe nazo. Sitashirikiana nawe kumtesa maskini kizuka na mayatima wake. (Anasema huku akiinuka na kuondoka)
1. Sehemu kubwa ya mazungumzo haya ilitokea wapi?
2. Ni sahihi kusema, Ponda na Adili:
3. Ponda angemwitaje Lulu?
4. Ni kweli kusema:
5. Unajua penye urembo ndipo penye uvimbo, maana yake ni:
6. Mumewe Lulu alikuwa nani?
7. Ponda alidai kuingilia kati mambo ya Lulu ili anufaishe nani?
8. Kisa hiki kinaashiria nini?
9. Kwa nini Adili akauita ufisadi saratani?