Kifungu cha 16

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yafuatayo.

Mnamo mwaka wa elfu moja mia kenda kumi na nne, vita vya kwanza vya ulimwengu vilizuka. Kwa mara nyingine tena na kwa bidii zaidi, binadamu alidhihirisha unyama wake licha ya kujidai eti ni muungwana na kiumbe razini. Mataifa yalitumia njenje tumbi nzima katika pilkapilka za kuyaangamiza mataifa mengine. Miradi mbalimbali ya kuinua kiwango cha maisha ya raia iliwekwa kiporo. Vita vikapewa kipaumbele. Zana za vita zikanunuliwa. Vijana kwa wazee, wakashirikishwa katika vita. Wengi wao hawakuyalalia wala kuyaamkia mambo yale. Wakawa tu ni bendera ifuatayo upepo. Hawakuelewa sababu ya wao kupigana. Wachache waliouliza walipata jawabu moja tu: “kutetea uzalendo, ufanisi na uungwana wetu.” Hawakujuta mbona wawachinje wenzao kama wanyama. Hawakuaibika mbona washangilie ndugu zao wanapoangamizwa kwa makombora. Mungu mwema tunusuru!

Hakuna refu lisilo na ncha. Mnamo mwaka wa elfu moja mia kenda kumi na tisa, vita vya kwanza vya ulimwengu vikafikia kikomo. Amani ikarejelewa. Mahasimu wakawa masahibu tena. Watu wakakumbatiana, tabasamu zikatawala nyusoni mwa wengi. Watu hata wakasameheana. Ikasemekana kuwa watu waishi kama ndugu wala sio kama hayawani. Ligi ya Mataifa ikabuniwa. Dhibitisho na ushuhuda kuwa hali imetulia na uadui umezikwa katika kaburi la sahau. Ushirikiano ukapishwa. Ukawa ni mwamko mpya. Ukawa ni wakati wa kukarabati. Watu wakajaribu kujenga upya yale waliyobomoa. Waliona ugumu kufanya yale lakini wakajikaza kisabuni. Ulikuwa ni mwiba wa kujidunga, nao hauna kilio. Lo! Kumbe ile amani ilikuwa ni hadaa ya jua wakati wa masika! Kumbe unafiki na uadui haukuwa umeangamia! Kumbe tabasamu zilikuwa zile za fisi mbele ya mbuzi! Kisasi kilikuwa bado kipo.

Ndoto za misingi ya ubinafsi bado zilikuwa zimejibanza na kuganda nyoyoni mwa wengi. Kumbe wahenga hawakutupatia ulimi wa kulazia walipoamba kuwa moyo wa mtu ni gongo la msitu! Mwaka wa elfu moja mia kenda arubaini na tano, maji yalizidi unga. Binadamu akavua nguo ya uungwana bandia na kuvaa johali ya ukatili na ubinafsi. Vita vya pili vya dunia vikazuka. Tamaa ya wapenda amani ikatamauka. Ndoto zao za amani zikayeyuka kama barafu motoni. Mwangaza wa utu ukafunikwa na giza la uhayawani. Wanyama waliokuwa katika ngozi za binadamu wakasababisha maafa ya kutisha usoni mwa dunia. Baada ya miaka minne, ikasemekana eti mshindi amepatikana. Vita vikafikia tamati. Lakini matatizo yakadumu hata leo. Ahadi zikatolewa. Dunia iwe ni mahali mwa amani. Hata umoja wa mataifa ukabuniwa.

Kisa na maana; kuhakikisha amani imedumu. Lakini swali ni hili. Je, amani imedumu? Vita vya wenyewe kwa wenyewe bado vinasikika. Taifa moja kulivamia jingine si jambo nadra wala adimu. Je, ina maana kuwa binadamu licha ya kutunukiwa akili kiasi hiki hawezi kutangamana na mwenzake kwa amani na heshima? Je, sharti mtu aonyeshe ufanisi na weledi wake kwa kuwagandamiza wenzake? Wakati ni sasa wa kuleta amani ya kudumu duniani. Tujiepushe na unafiki. Tusiwe ndumakuwili. Hakuna haja ya kuandaa mikutano eti kuzungumzia amani ilhali washiriki na washikadau wana nia nyingine nyoyoni mwao. Tabasamu na kukumbatiana mbele ya kamera si chochote si lolote ikiwa nyoyoni mmejaa vifundo vya uhasama. Amani ya kweli haitatokana na mikutano bali uwazi, huruma, heshima na mapenzi.Tujitahidi kupata suluhisho kwani bado tunaishi chini ya kivuli cha aibu ya vita viwili vilivyotangulia. Hatutaki vita vingine. Hivyo viliathiri dunia vya kutosha.

Maelezo ya msamiati

  • razini – -enye akili timamu, -enye uwezo wa kufikiri
  • weledi – wajuzi, wenye ujuzi

1. Kulingana na taarifa, ni maelezo yapi sahihi?        

  1.  Kabla ya mwaka wa elfu moja mia kenda kumi na nne, ulimwengu haukuwa na vita      vyovyote.
  2.  Vita vya kwanza vya dunia viliisha kwa kubuniwa kwa Umoja wa Mataifa.
  3.  Vita vya kwanza vya ulimwengu vilichukua miaka minne kumalizika.    
  4.  Vita vya kwanza vya ulimwengu vilisababisha maafa makubwa.

2. Ni kweli kusema:      

  1.  washirika wote katika vita vya kwanza vya dunia hawakuelewa sababu ya vita hivyo.          
  2. Vita vya kwanza vya dunia vilisababishwa na uungwana.
  3.  Vita vya kwanza vya ulimwengu vilisababishwa na utetezi wa uzalendo, ungwana na ufanisi.                                                                                                  
  4. Vita vya kwanza vya ulimwengu vilisababishwa na ubinafsi.

3. Unafikiri ni kwa nini watu hawakujali maisha ya wenzao?  

  1. Walikuwa na chuki na ubinafsi. 
  2. Hawakuwaona wenzao wakiteseka.   
  3. Hawakuwa na uwezo wa kuwasaidia.   
  4. Walikuwa wazalendo.

4. Kumbe ile imani ilikuwa ni hadaa ya jua wakati wa masika! Ina maana kuwa:  

  1. Amani ingedumu kwa muda mrefu.  
  2. Amani ingeisha wakati wa masika.          
  3. Amani ile haingedumu sana.                    
  4. Watu wangedumisha amani.

5. Ni lipi lililokuwa dhibitisho la kupatikana kwa amani baada ya vita?  

 

  1.   Kubuniwa kwa ligi ya mataifa.  
  2.   Kukumbatiana kwa wapiganaji.    
  3.    Kubuniwa kwa Ligi ya Mataifa pamoja na Umoja wa Mataifa.      
  4.    Kupatikana kwa mshindi.

6. moyo wa mtu ni gongo la msitu ina maana:

  1.   Moyo wa mtu una giza kubwa. 
  2.  Si rahisi kujua siri zilizo moyoni mwa mwenzako.
  3. Moyo wa mtu ni katili.                            
  4.  Moyo wa mtu una hatari nyingi.

7. Tamaa ya waashiki wa amani ilitamauka lini?        

  1.   Vita vya kwanza vya ulimwengu vilipoanza.
  2.  Vita vya pili vya ulimwengu vilipoanza. 
  3. Watu walipoanza kulaumiana.                    
  4. Mshindi alipopatikana.                             

8. Ni sentensi ipi sahihi?  

  1. Vita vya kwanza na vya pili vya Dunia vilidumu kwa wakati sawa.  
  2.  Vita vya pili vya Dunia vilipiganwa wakati wa usiku.      
  3.   Mwisho wa vita vya pili vya Dunia uliipisha amani ya kudumu kote duniani.  
  4.   Kuisha kwa vita vyote viwili hakujabadilisha mambo sana duniani.

9. Kwa nini mwandishi anawafananisha watu waliohusika katika vita na wanyama?

  1.  Anawachukia.
  2.   Hawakuonyesha utu katika matendo yao.  
  3.   Walikuwa wakali sana.        
  4.   Walikuwa wakipigana huko msituni.                                      

10. bado tunaishi chini ya kivuli cha aibu ya vita viwili vilivyotangulia.. Mwandishi anakusudia kusema nini?  

  1. Bado athari za vita hivyo havijaangamia.    
  2.  Bado amani haijapatikana.            
  3.  Bado watu hawajaonyesha uungwana.  
  4.   Bado hatujapata suluhisho.