Kifungu cha kumi na tatu Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Kutojua na kupuuza ni mambo mawili tofauti. Hata hivyo, yote ni pingamizi kwa ufanisi wowote ule. Kutojua ni ile hali ya kutoelewa jambo. Labda mja hana nafasi au uwezo wa kuling’amua jambo fulani. Kupuuza ni hali ya kuwa na nafasi na uwezo wa kulielewa jambo lakini mja akakataa kulielewa. Labda akaona halina umuhimu wowote ule. Ni saratani mbaya zaidi. Ni kiini cha maafa duniani. Huenda mja akasamehewa hata kuonewa shufaka kwa kutojua. Lakini kwa vyovyote vile, mja awaye yule hawezi kusamehewa kwa kupuuza. Badala yake, atachekwa na aonekane mshenzi. Huenda akakumbushwa kuwa, mwiba wa kujidunga haustahili pole. Mtoto akizaliwa, huwa hajui hali ya dunia. Halijui baya wala zuri.
Polepole jinsi anavyozidi kukua, dunia nayo inanyoosha mikono kumpokea. Dunia hii ya binadamu katili humfundisha mengi, mema kwa mabaya. Ni jukumu lake kuyaelewa yote anayofundishwa. Ayafuate yaliyo adili na ayatupilie mbali yaliyo ayari. Mtoto atasamehewa asipoyafanya yaliyo mema iwapo tu hajafundishwa kupambanua mazuri na mabaya. Wakati huo watu watasema kuwa anakosa kwa kutojua. Afundishwapo mema na kutahadharishwa kutotenda yasiyofaa, kisha ayatende, atasemekana ni mpuuzaji. Kisa na maana, ameyapuuza mafunzo ambayo ameshapewa. Hilo linapotokea, ili maji yasizidi unga, ili kukiwahi chuma kingali moto, adhabu na nasaha hazina budi kutolewa. Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya watu ambao hulaumiwa eti ni wapuuzaji ilhali ukweli ni kwamba hawajui. Ni wajinga wa jambo lile. Hawakufundishwa. Badala ya kuwalaumu wasiojua, yafaa tuwafundishe na kuwashauri. Huenda makosa si yao.
Ni ya wale waliokuwa na jukumu la kuwafundisha lakini wakapuuza wajibu wao. Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa, duniani kuna insi tumbi nzima ambao hujipata makosani. Si kutokana na upuuzaji bali kwa kutojua. Ukweli ni kuwa, yupo mtu au watu waliopuuza jukumu lao la kuwaelimisha na kuwashauri. Kwa bahati mbaya, aghlabu mtu anapokosa, dunia haiangalii iwapo amekosa kwa kutojua au kwa kupuuza. Dunia hukimbilia uamuzi mmoja tu. Amekosa kwa kupuuza. Ninafikiri hili ni tatizo kubwa kwa dunia nzima kwani tabia hiyo ya kukimbilia uamuzi pasi uchunguzi ni ishara ya upuuzaji kwa wahusika.
Maelezo ya msamiati
1. Ni maelezo yapi sahihi kulingana na kifungu?
2. Ni nani anayestahili kulaumiwa iwapo mtoto hajui mambo anayotakikana kuya jua?
3. Mtoto anapokosa, anastahili:
4. Mpuuzaji kwa kawaida:
5. … maji yasizidi unga inamaanisha:
6. Mtu asipofundishwa jambo, yeye ni:
7. Makosa ya dunia ni yapi?
8. Upuuzaji na ujinga utaisha iwapo:
9. Tabia ya kukimbilia uamuzi bila kuchunguza kikamilifu ni ishara ya:
10. Methali ipi mwafaka kuelezea maafa ya upuuzaji?