Kifungu cha kumi: Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yatakayofuatia
Mzaha mzaha hutunga usaha. Nao usaha hunuka na una aibu. Aibu nayo huleta majuto na kushuka kwa heshima. Afanyaye jambo lenye aibu haheshimiki. Kwa miaka ayami, wimbo wa uhifadhi wa mazingira umekuwa vinywani mwa wengi. Kila kukicha tukaelezewa tujiepushe na ukataji ovyo wa miti. Tukahimizwa na kuelimishwa kuwa iwapo tutaikata miti, basi tuipande mingine papo hapo. Tulielezwa tele kuhusiana na utumiaji mbolea asilia ambayo haina madhara katika udongo wetu. Hatukukosa wosia na nasaha kuhusiana na mbinu mwafaka za kilimo ili kuepuka au kuzuia mmomonyoko wa udongo. Lakini yote hayo, wengi wetu tuliyatemea mate. Ikawa ni sawa na kumwashia kipofu taa. Ni sawa na kumpigia mbuzi gita. Tulishauriwa kutoichafua mito yetu lakini tukaigeuza kuwa mabomba ya uchafu.
Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wawekezaji wakielekeza mifereji ya maji taka kutokaviwandani mwao hadi mitoni au maziwani. Si ajabu tena kuona mifereji kutoka vyooni ikielekezwa hadi mitoni. Isisahaulike maji ya mito yiyo hiyo yanatumiwa na binadamu, mifugo, ndege na wanyamapori. Ukizuru mitaa yetu, utashangaa kuona kuwa, nusura katika kila sehemu wazi, imegeuzwa kuwa biwi la takataka. Mirundiko ya takataka inayonuka fee imesimama kwa aibu kila mahali. Ni aibu na fedheha yetu hiyo. Kivuli hicho cha fedheha kinatuandama popote tuendapo licha ya kujiita wastaarabu na wajuaji. Matokeo ya hayo yote ni masaibu tele yanayotufuata. Hatuachi kulalamika kutokana na maradhi ya kila aina. Tutaepukaje maradhi ilhali baadhi ya mboga tunazotumia hunyunyiziwa maji ya takataka! Maradhi yatokanayo na uchafuzi wa hewa limekuwa jambo la kawaida aushini mwetu.
Mikurupuko ya ndwele kama vile kupindupindu si jambo geni maishani mwetu. Kweli usaha hunuka. Nayo majuto ni mjukuu mwishowe huja kinyume. Uhaba wa chakula ni tisho kubwa kwetu. Kutokana na mbinu mbovu za kilimo, mashamba yetu yanazidi kushindwa kutosheleza mahitaji yetu. Mito yetu nayo inazidi kukauka. Viumbe vya majini vinazidi kudidimia. Kisa na maana, misitu inazidi kudidimia nayo mito inazidi kuchafuliwa. Mingi yao inaweza kuitwa mito ya sumu. Maafa hayo yote yanatokana na miaka mingi ya mzaha. Mzaha dhidi ya mazingira yetu. Mambo ambayo yanastahili kuchukuliwa kwa uzito ufaao tukayadhararisha. Nayo matokeo ndiyo haya. Maafa yanayotishia sio maisha yetu tu bali na ya vizazi vijavyo. Yafaa tuchukue hatua mwafaka, imara na za dharura. Tuirejeshe hali ya zamani ili tuweze kufurahia mandhari yetu.
Maelezo ya msamiati
1. Kulingana na kifungu, majuto hutokana na:
2. Kwa nini mwandishi anafananisha hali husika na kuwashia kipofu taa?
3. Kulingana na ufahamu, mmomonyoko wa udongo husababishwa na:
4. Mirundiko ya takataka … imesimama kwa aibu, inamaanisha:
5. Kwa nini mwandishi anasema, majuto ni mjukuu?
6. Ukataji ovyo wa miti husababisha yafuatayo ila:
7. Ni yapi matokeo ya uchafuzi wa mazingira?
8. Tatizo la mazingira linatishia:
9. Mandhari ina maana ya:
10. Ufahamu huu unatoa ujumbe upi?