Kifungu cha 9

Kifungu cha tisa Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yatakayofuatia  

Boka alijishika tama, akaangalia viambaza vya seli ile. Matumaini yake yakazidi kudidimia. Lililompotezea matumaini zaidi ni vile vikuku vilivyokuwa viwikoni mwa mikono yake. Hiyo ilikuwa ni siku ya kukatwa kwa kesi yake. Alikuwa katika seli ya mahakama chini ya ulinzi mkali. Kwa miaka miwili mtawalia, alikuwa katika rumande. Siku hiyo hakutarajia mageni. Iwapo angebahatika, basi angeepuka na kifungo kirefu au hata cha maisha gerezani. Na iwapo asingebahatika basi, angehukumiwa kula kitanzi kutokana na kosa la wizi wa mabavu. Kwa miezi ishirini na minne, mawakili wake walijaribu juu chini kumtetea bila kufanikiwa. Jaribio lao la kutaka mteja wao aachiliwe kwa dhamana halikadhalika liligonga mwamba. Licha ya kuwa na njenje chungu nzima, alizochuma kwa njia za haramu, alishindwa kuupata uhuru wake.

Hapo ndipo alipong’amua kuwa pesa si kila kitu. Ingawa pesa huvunja milima na nguu kulala, mara kwa mara, nguu nyingine hughairi pesa. Wazo la kujiona pale kizimbani huku hakimu akitoa hukumu lilimsababishia Boka tumbo la kuendesha. Alinyanyuka polepole hadi pale ndooni. Kwa ugumu mwingi aliweza kwenda haja kisha akarejea pale pale pembeni. Alizivuta nyuma fikra zake na kujuta jinsi alivyopotoka. Kimzaha tu, alianza kuwa kichwa maji pale shuleni. Polepole akawa mtoto asiyelika wala kutafunika. Aliwatesa na kuwachapa maghulamu wa rika lake kiasi cha kupata msimbo ‘Moto’. Alikumbuka jinsi alivyoanza uraibu wa kutumia sigara kimchezo tu kisha akahitimu na kujiunga na chuo cha uvutaji bangi. Nao uvutaji bangi ukampatia msisimko wa ajabu. Mambo yote kwake akayaona ni mboga.

Akapata ujasiri wa ajabu kiasi cha kuhisi kuwa angepigana na bila shaka amshinde yeyote yule. Hata simba mfalme wa nyika! Machozi yalimdondoka alipokumbuka jinsi elimu yake ilivyokatika. Akakumbuka jinsi kipaji chake katika mchezo wa soka kilivyoangamia. Kiamboni nako wakawa hawasikizani na yeyote. Si wavyele si umbu zake. Shuleni mambo yakawa ni yayo hayo. Mambo yaliwafika walimu kooni alipogeuka na kuwa tisho kwa usalama na maisha ya walimu. Alikumbuka kwa masikitiko tele jinsi alivyojaribu kumdunga kwa kisu mwalimu wake wa Kiswahili. Kisa na maana, maskini mwalimu alipojaribu kufafanua methali “mkataa ya mkuu huona makuu”. Boka alidai mwalimu wake alikuwa akimpiga vijembe. Kwa nyota ya jaha, mwalimu yule aliupata upenu na kusema mguu niponye na kuyaokoa maisha yake.

Alipotimuliwa shuleni, alielekea mjini. Huko alipatana na wenzake masikio ya kufa. Kwa miaka minne, waliwasumbua wananchi wapenda amani. Walivuna kule ambako hawakupanda wala kupalilia. Kutokana na matendo yao, wakachuma pesa vilivyo na wakaishi maisha ya anasa. Siku za mwizi ni arobaini. Siku moja walifumaniwa wakiiba katika dukakuu moja. Wanne walisalimu amri mbele ya bunduki. Boka alipoona hayo, alibwaga silaha na kujisalimisha.

Maelezo ya msamiati                                                                                                                      viwikoni – mkononi panapounganisha kiganja na sehemu ya juu ya mkono  

  • njenje – pesa
  • kizimbani – sehemu ya mahakamani
  • msimbo – lakabu; jina la kubandikwa
  • upenu – mwanya, nafasi ndogo

 

1. Kitendo cha kujishika tama kinaashiria hali ipi ya mhusika?

  1. Huzuni          
  2. Wasiwasi            
  3. Hasira              
  4. . Majuto

2. Siku hiyo, hakutarajia mageni inamaanisha:  

  1. siku hiyo hangepata wageni.      
  2. siku hiyo hangehukumiwa.                
  3. siku hiyo hangepata uhuru.        
  4. siku hiyo angeachiliwa huru.

3. Kwa nini Boka alienda haja kwa ugumu mwingi?

  1. Alikuwa mgonjwa.         
  2. Alikuwa na pingu mikononi.  
  3. Alikuwa amechoka.     
  4. Ndoo ilikuwa ndogo.

4. Ni wakati upi Boka aliacha kuzithamini pesa kupita kiasi?  

  1. Alipokuwa shuleni.    
  2. Alipotiwa mbaroni.               
  3. Aliposhindwa kutoka rumande.      
  4. Alipofikishwa mahakamani.

5. Boka alianza kwenda kombo lini?            

  1.   Alipokutana na vijana wezi.          
  2.   Alipoanza kutumia bangi.                        
  3.   Alipomshambulia mwalimu wake.    
  4.    Alipoanza kuwakaidi walimu shuleni.

6. Ni yapi yaliyosababisha Boka kulia?    

  1.  Mateso ya gerezani.              
  2.  Hukumu ya kifungo kirefu gerezani.                    
  3.   Majuto ya kuupoteza ujana wake.  
  4.   Hasira za kutiwa mbaroni.

7. Ni maelezo yapi sahihi?  

  1.  Boka aliponea chupuchupu kupigwa risasi na askari.    
  2.  Wenzake Boka waliweza kutoroka askari.        
  3.  Boka alimdunga kwa kisu mwalimu wake.
  4.   Boka alitoroka shuleni kuepuka adhabu.

8. Ni yapi yaliyomwokoa mwalimu wa Kiswahili?  

  1. Mbio zake.    
  2. Upenu uliokuwa pale karibu.   
  3. Mayowe ya walimu wenzake.    
  4. Nyota ya jaha.

9. Ni nini maana ya umbu katika kifungu?  

  1. Rafiki.         
  2. Wavyele.    
  3. Ndugu.            
  4.  Walimu

10. Toa kichwa mwafaka zaidi kwa hadithi hii.      

  1.   Boka na wenzake.  
  2.   Hukumu kali.    
  3.   Majuto ni mjukuu.  
  4.   Kifungo cha Boka.