Kifungu cha 7

Kifungu cha saba: Soma kifungu kifuatacho ili ujibu maswali yatakayofuatia.

Tuliiongoza mifugo yetu hadi malishoni. Ulikuwa ni msimu wa kiangazi nalo jua lilikuwa la mtikati. Sote tulikuwa ni maghulamu wa hirimu moja. Kiranja wetu alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu. Baada ya kuichunga mifugo kwa saa mbili hivi, tuliamua kwenda kuogelea katika kijiziwa kilichokuwa kitalifa kifupi kutoka hapo machungani. Ilitubidi tuiache mifugo pale mikononi mwa mmoja wetu. Hakuna aliyejitolea kubaki. Sote tulitaka kwenda kuogelea. Lisilo budi hubidi. Tulikata shauri kupiga kura. Tulipiga kura na Musa akawa ndiye angeichunga mifugo. Tuling’oa nanga kwa vicheko huku tukimwacha Musa katika hali ya huzuni na upweke. Tulimpa pole za bandia huku tukimcheka kisirisiri. Wengine walisikika wakimfanyia mzaha kuwa wangempelekea maji aogelee pale malishoni wakati wa kurejea.

Kwa mara ya kwanza, nilijigeuza kuwa maji yafuatayo mkondo. Niliyatemea mate maonyo ya mamangu. Tuliandamana na wenzangu moja kwa moja kuelekea kiziwani. Kitambo tufike, tuliamua kupitia shambani mwa Mzee Kaumu. Konde lake lilijaa mihogo. Tuliivamia kwa uroho uliopita ule wa fisi. Dakika chache baadaye, tulikuwa njiani kuelekea kiziwani tayari kuogelea. Ungetusikia ungesamehewa iwapo ungedhani ni kundi la fisi kutokana na vicheko tulivyoangua. Tulifika kiziwani na kuanza kuogelea. Kila samaki alitaka kudhihirisha ubingwa wake. Wajuzi walipiga mbizi kwa ustadi mkuu. Wengine kama mimi, tulijirushiarushia maji kandokando ya kiziwa. Mtu hujikuna ajipatapo. Aidha, ukimwiga tembo kunya utapasuka …. Nilidhamiria kurejea kiamboni nikiwa mzima. Hata wanagenzi kama mimi, baadaye tulitekwa bakunja na uogeleaji. Tulipotanabahi, giza lilikuwa likibisha hodi. Mbiombio tulielekea tulipoziweka lebasi zetu. La ajabu, hata Musa alikuwa kati yetu.

Hakuna aliyemwuliza mbona akaja au ilikokuwa mifugo kwani maajabu mengine yalitukodolea macho.. Nguo zetu hazikuwepo. Mungu mwema! Tuliangaliana bila kusema lolote. Hakuna aliyetaka kusema alilofikiria. Tukiwa katika hali ya kuchanganyikiwa, tulisubiri hadi giza lilipotanda. Si wahenga walisema usiku ni lebasi bora? Tulifika kiamboni baada ya safari ya tahadhari kuu kupitia vichakani. Kiamboni nilikuta mengine. Mmiliki wa shamba la mihindi lililopakana na malishoni alikuwa pale machozi yakimdondoka. Mazao yake yote yalikuwa yameangamizwa na mifugo yetu. Mzee Kaumu alikuwa pale akililia damu yetu. Kumbe tayari alikuwa ameiuza mihogo ile! Angemwelezaje mteja wake? Yaliyonipata jioni hiyo mikononi mwa mama, sidhani yatafutika akilini mwangu. Kwa njia moja au nyingine yalikuwa ni dira ya maisha yangu. La sivyo, labda leo hii ningekuwa kinyangarika, mkia wa mbuzi.

Maelezo ya msamiati

  • kitalifa – umbali
  • kiamboni – nyumbani
  • uroho – tamaa l
  • ebasi – nguo
  • tekwa bakunja – pumbazwa na jambo
  • kinyang’arika – mtu asiye na thamana

1. Mwandishi wa makala haya alikuwa na umri wa:  

  1.  takribani miaka kumi na mitatu.      
  2.  hirimu.      
  3.  makamo.      
  4.  uzee.

2. Kwa nini wahusika walipiga kura?      

  1.  Walitaka mcheka yule angebaki na mifugo.    
  2.  Walikuwa wamekosa kukubaliana yupi kati yao angebaki na mifugo.            
  3.  Walitaka kuogelea.
  4. Walikuwa na nia ya kumchagua kiranja wao.

3. Ni kweli kusema:  

  1. Musa alifurahia matokeo ya kura.        
  2. Wenzake Musa walimwonea huruma.    
  3. Wenzake Musa walimtania.                              
  4. d. Kamwe Musa hakuenda kuogelea.  

4. Kwa kawaida, tabia ya mwandishi ilikuwa:  

  1. ya utundu na utukutu.              
  2. ya utiifu na uajibikaji.                  
  3. ya uzembe na mabezo.                              
  4. ni vigumu kueleza.

5. Maelezo yapi sahihi?

  1. alimiliki shamba la mahindi.    
  2. Wahusika walienda kuogelea mwendo wa alasiri.
  3. Mwandishi alikuwa gwiji wa kuogelea.  
  4. Mzee Kaumu alikuwa akilia.

6. Ukimwiga tembo kunya utapasuka…. Kulingana na kifungu, maelezo haya yanamaanisha:  

  1.  Mwandishi hakuwaiga waliojua kuogelea.        
  2.  Mwandishi alishindana na wenzake kuogelea.  
  3.  Mwandishi alikuwa mwoga wa kuogelea.    
  4.   Mwandishi alikuwa mwangalifu asishindwe na wenzake.

7. Yaelekea ni nani aliyeipeleka mifugo kiamboni?    

  1.  Musa      
  2. Kaumu    
  3. Mmiliki wa shamba la mahindi    
  4. Mifugo ilijipeleka yenyewe

 

8. Kwa nini wenzake Musa hawakumwuliza kuhusu mifugo?

  1. Walimwogopa.          
  2.  Walimwonea huruma.            
  3.  Walichanganyikiwa kwa kuchelewa.    
  4.   Walichanganyikiwa kwa kushindwa wangevaa nini.

9. Kwa nini wahusika walisubiri giza litande?  

  1.  Ili wasionekane na mwenye shamba.  
  2.  Ili wapate watu wamelala.                      
  3.  Ili waweze kutembea hadi nyumbani.        
  4. Ili wasionekane na watu wakiwa uchi.

10. Ni kweli kusema:              

  1.    Mwandishi hajutii adhabu aliyopata.      
  2.    Mwandishi hakuadhibiwa.              
  3.    Mwandishi hafurahishwi na adhabu aliyoipata.  
  4.    Mwandishi ashaaisahau nidhamu aliyoipata.