Kifungu cha tano: Soma barua ifuatayo kisha ujibu maswali yatakayofuatia.
Kaya ya Uwezo, S.L.P 2001, MARAGWA. 20.7.04. Kwa kaka, Kwanza zipokee salamu tumbi nzima kutoka kwetu huku Kiamboni. Sisi hatuna neno ila tu kulisukuma gurudumu la maisha. Ni matumaini yangu kuwa hata wewe huko uliko ughaibuni u salama salimini na mwenye buheri wa afya. Nimekata shauri kukuandikia waraka huu kwani wahenga na wahenguzi hawakutupiga mafamba walipoamba kuwa, barua ni nusu ya kuonana. Kaka, lengo la kukuandikia waraka huu ni kukueleza hali ya mambo hapa mastakimuni. Mambo hapa ni tele. Mengine mazuri ilhali mengine ni vioja na viroja. Ni ya kuatua moyo. Ninayo furaha ghaya kukujulisha kuwa dadetu Subira alifua dafu kufunga pingu za maisha. Alifunga nikahi na shababi mmoja mtanashati ajabu na mwenye heshima zake.
Ama kweli mvumilivu hula mbivu. Licha ya kuchekwa na kupigwa vijembe na mabanati wenzake, Mungu alimjalia mume wake. Nalo la wahenga likatimia Mola hamwachi mja wake na asiye na wake ana Mungu. Aidha, nina naye alipandishwa mamlaka kazini kutokana na bidii zake. Alipandishwa ngazi moja na kuwa Mwalimu Mkuu shuleni mwao. Hilo nalo lilitufurahisha si haba. Waama, bidii hulipa na chanda chema huvishwa pete. Baba naye alifua dafu kununua rukwama. Rukwama hiyo anaitumia katika harakati zake za uhamali kila siku za Jumatano na Jumamosi. Yeye hubebea wanakaria mizigo yao hadi cheteni. Hata hivyo, ninasikitika kukueleza kuwa, babu bado hajaona ashekali. Bado uwele wake unazidi kuwafanyia matabibu mzaha. Tumempeleka kwa waganga na waganguzi lakini yote ni bure bilashi! Yote yanaonekana sawa na kukimbizana na upepo.
Je, kaka, unamkumbuka jirani yetu Kiu? Siku hizi yeye si hayati si mamati. Yu katika pumzi zake za mwisho. Maskini Kiu alichezea tope na bila shaka likatimia la wahenga kuwa mchezea tope huchafuka. Katika shughuli zake za anasa, aliambukizwa virusi vya ukimwi. La kuhuzunisha zaidi ni kuwa, hata ahali wake pia ni mgonjwa. Alimwambukiza. Kwa kweli, mchuma janga hula na wa kwao. Mjomba Mkono naye alihukumiwa kula kalenda gerezani. Alifumaniwa akimwibia ajuza mmoja katika kijiji jirani. Wanakijiji walipandwa na mori na kumpiga kitutu. Ni bahati tu, hakuelekezwa jongomeo. Mbali na kufungwa gerezani kifungo kirefu, alilemazwa kwa kuvunjwa miguu yake miwili na kung’olewa jicho. Ni kweli tamaa mbele mauti nyuma. Janga la gharika aidha limewakumba wakazi wa kijiji jirani.
Kwa mara nyingine tena, mto Pigo umevunja kingo zake na kusambaza hasira zake makondeni mwa wakulima. Hali hiyo imeathiri pilkapilka zao za zaraa. Nao ugemaji na ulevi wa pombe haramu unazidi kuangamiza wengi. Vijana kwa wazee hawajaepuka wimbi hili la maangamizi. Hivi majuzi, wanakijiji endashara walienda kuzimuni huku korija moja wakipofuka macho kutokana na ulevi wa mvinyo haramu. Kasi, mzuwanda wetu, juzi aliona kilichomfanya sangara achomwe moto Alitiwa mbaroni na maafisa wa usalama barabarani kwa kudandia kwenye matwana. Mahakamani alihukumiwa kutoa faini kwa kutozingatia sheria za barabarani. Ndugu mpendwa, kwa sasa sina nyongeza. Wasalimie wasena wako huko uliko. Wavyele , ndugu zangu na jirani wamekusalimia sana. Nyanya amenieleza nikukumbushe kuwa mwacha mila ni mtumwa. Usiyaige ya ugenini bila tahadhari. Aidha, elewa ukimwi upo.Jihadhari kwani hasara humfika mwenye mabezo na mchezea mavi hunuka.
Kazole ya heri.
Ndugu yako wa toka nitoke, Saba Nane Kipande.
Maelezo ya msamiati
1. Lengo kuu la mwandishi kumwandikia kakaye lilikuwa lipi?
2. Kwa nini mwandishi anayo furaha ghaya?
3. Kulingana na mwandishi, hapo awali mama yake alikuwa na hadhi ipi kazini?
4. Ni maelezo yapi sahihi zaidi kulingana na barua hii?
5. Ni sahihi kusema:
6. Kitendo kinachoonyesha ukweli wa methali mchuma janga hula na wa kwao ni:
7. Teua maelezo sahihi kulingana na kifungu.
8. Maelezo yapi ni sahihi?
9. Mauti ya watu endashara yalisababishwa na:
10. Mwandikiwa anajishughulisha na yapi huko ughaibuni? a. Masomo.