Ushairi

Ushairi

Ni sanaa ya utunzi wa shairi. Shairi ni mtungo wa kisanaa ambao hufuata sheria fulani kama vile ukataji wa maneno. Mtu atungaye shairi huitwa malenga.

Aina/bahari za shairi

Mashairi hutajwa kulingana na yafuatayo:

  • Urefu na mada ya shairi k.m. shairi refu ambalo linaelezea historia au kisa fulani huitwa utenzi.
  •  Washiriki katika shairi k.m shairi la kujibizana baina ya watu wawili au zaidi huitwa ngonjera au malumbano.
  •  Idadi ya mishororo (mistari) katika kila ubeti:

Tathmina – shairi lenye mshororo mmoja katika kila ubeti

Tathnia – shairi lenye mishororo miwili katika kila ubeti.

Tathlitha – shairi lenye mishororo mitatu katika kila ubeti.

Tarbia – shairi lenye mishororo minne katika kila ubeti.

Takhmisa – shairi lenye mishororo mitano katika kila ubeti.

Tashlitha – shairi lenye mishororo sita katika kila ubeti.

Usaba – shairi lenye mishororo saba katika kila ubeti.

Tasdisa – shairi lenye mishororo tisa katika kila ubeti

Ukumi – shairi lenye mishororo kumi katika kila ubeti 

Shairi huwa limegawika katika mafungu kadhaa yaitwayo:

Ubeti ni kifungu cha maneno katika shairi. ubeti (umoja), beti (wingi). Ubeti nao huwa umegawika katika mistari iitwayo mishororo. Unaweza kufananisha ubeti na aya katika hadithi. k.m                                                                                                                                                       Ubeti: Zishikeni zenu ndewe, kwa yakini niwambie (mshororo) Rabuka muumba wewe, kaniumba pia mie (mshororo) Mbona ndugu tujigawe, kabila tujigawie? (mshororo) Twajipalia makaa, polepole twajioka. (mshororo)

Mishororo Kila mshoro ro katika ubeti unalo jina lake k.v:                                                      

  1.   Mwanzo – Mshororo wa kwanza katika kila ubeti.
  2. Mloto – mshororo wa pili katika kila ubeti.
  3. Mleo – mshororo wa tatu katika kila ubeti.
  4.  Kituo – mshororo wa mwisho katika kila ubeti.

Mshororo wa nne au mwisho katika ubeti ambao unarudiwarudiwa una majina yafuatayo:

kipokeo, kiitikio, mkarara, kibwagizo.

Mshororo wa mwisho ambao haurudiwirudiwi huitwa: kimalizio, kiishio.

Mfano:

Zishikeni zenu ndewe, kwa yakini niwambie (mwanzo)

Rabuka muumba wewe, kaniumba pia mie (mloto)

Mbona ndugu tujigawe, kabila tujigawie? (mleo)

Twajipalia makaa, polepole twajioka. (kibwagizo)

Kibarua ukitaka, huna budi tambuliko (mwanzo)

Kwa kabila kujulika, ujulike utokako (mloto)

Majina yasoeleka, ni patupu ambuliko (mleo)

Twajipalia makaa, polepole twajioka. (kibwagizo)

Sehemu za mishororo Sehemu katika mshororo huitwa kipande. k.m Zishikeni zenu ndewe, kwa yakini niwambie 1 2 Hivi ni vipande viwili. Kipande cha kwanza huitwa ukwapi, cha pili ni utao ilhali cha tatu ni mwandamizi.

Shairi ambalo limegawika katika ukwapi na utao huitwa manthawi.

Mfano

Zishikeni zenu ndewe, kwa yakini niwambie ukwapi utao

Rabuka muumba wewe, kaniumba pia mie ukwapi utao

Mbona ndugu tujigawe, kabila tujigawie? ukwapi utao

Twajipalia makaa, polepole twajioka. ukwapi utao

Silabi Silabi ni sehemu ya neno ambayo hutamkwa pamoja kama fungu moja la sauti. k.m. “ka” na “ta”

Katika neno “kata” zipo silabi mbili tofauti. Kwa hivyo, neno kata lina silabi mbili nazo ni “ka” na “ta”.

Mifano Neno Idadi ya silabi oa o-a 2 silabi si-la-bi 3 hutamkwa hu-ta-m-kwa 4 tuungane tu-u-nga-ne 4

Mizani

Mizani ni idadi ya silabi katika mshororo wa shairi au utenzi.

Mizani huweza kuwa ya silabi ya herufi tofauti:

  1.  moja kama a, e, i, o, u.
  2.  mbili kama ba, be, bi,
  3.  tatu kama bwa, bwe, bwi,
  4.  nne kama mbwa, mbwe, mbwi,

Kwa hivyo, ukiulizwa utaje mizani katika mshororo, ubeti au shairi lote, unahitaji kujumuisha silabi zote za maneno kwenye kifungu husika. k.m. Ubeti huu unayo mizani ngapi?

Zishikeni zenu ndewe, kwa yakini niwambie

Rabuka muumba wewe, kaniumba pia mie

Mbona ndugu tujigawe, kabila tujigawie?

Twajipalia makaa, polepole twajioka.

Jibu : Unazo mizani 64 (kama ilivyoonyeshwa)

Zi-shi-ke-ni ze-nu nde-we, kwa ya-ki-ni ni-wa-mbi-e – mizani 16

Ra-bu-ka mu-u-mba we-we, ka-ni-u-mba pi-a mi-e – mizani

16 Mbo-na ndu-gu tu-ji-ga-we, ka-bi-la tu-ji-ga-wi-e? – mizani

16 Twa-ji-pa-li-a ma-ka-a, po-le-po-le twa-ji-o-ka. – mizani 16

Jumla: Mizani 16 mara nne = mizani 64

Vina Silabi za mwisho wa maneno zinazofanana ambazo aghalabu hutokea katikati na mwisho wa vipande vya shairi huitwa vina (umoja: kina).

Silabi za mwisho katika ukwapi huitwa vina vya kwanza au vya kati.

Silabi za mwisho katika utao huitwa vina vya pili au vina vya mwisho.

Mf. K.m.

Zishikeni zenu ndewe, kwa yakini niwambie

Rabuka muumba wewe, kaniumba pia mie

Mbona ndugu tujigawe, kabila tujigawie?

Twajipalia makaa, polepole twajioka.

Vina vya kati – we, a

Vina vya mwisho – e, ka

Katika mambo ya ushairi kuna mbinu zinazotumika kama vile.

  1.  Urari ni mpangilio wa kueleweka wa vina, mizani na mishororo ya beti za shairi.
  2.  Mpangilio au mtiririko wa mawazo ya mshairi kutoka ubeti mmoja hadi mwingine huitwa muwala.
  3.  Inkisari ni mbinu ambapo mshairi huwa na uhuru wa kuyafupisha maneno ili kutosheleza vina/mizani ya mshororo k.m. babangu badala ya baba yangu.