Wakati
Wakati
Katika lugha ya Kiswahili tunazo nyakati mbalimbali. Nyakati hizi huwakilishwa kwa viambishi mbalimbali. Nyakati hizi huashiria majira au muda mbalimbali.
- Wakati uliopo (wakati wa leo) Kiwakilishi – n a – hutumika. k.m: Mtoto anacheza matopeni;
Wanafunzi wanasoma.
- Wakati uliopita (wakati wa jana) Kiwakilishi – l i – hutumika k.m. Mtoto alicheza matopeni; Wanafunzi walisoma.
- Wakati ujao (wakati wa kesho) Kiwakilishi – t a – hutumika k.m. Mtoto atacheza matopeni;Wanafunzi watasoma.
- Wakati wa mazoea (kila wakati) Kiwakilishi – h u – hutumika k.m. Mtoto hucheza matopeni; Wanafunzi husoma. Muhimu Katika wakati wa mazoea, kiwakilishi cha wakati ndicho hutangulia katika kitenzi. Kiwakilishi cha nafsi hakiwekwi kwenye kitenzi k.m. Mtoto husoma kwa bidii.
- Wakati uliotimia (timilifu). Wakati wa me. Kiwakilishi me hutumika k.m. Mtoto amecheza matopeni; Wanafunzi wamesoma.
- Wakati ujao kuendelea kwa kitendo Wakati huu huonyesha kuwa kitendo kitakuwa kikiendelea wakati ujao. -takuwa na ki– hutumika k.m Mtoto atakuwa akicheza matopeni; Kesho wanafunzi watakuwa wakisoma. Muhimu Ni makosa kutumia –takuwa pamoja na –na–. Mtoto atakuwa anacheza X
- Wakati uliopita hali ya kuendelea kwakitendo Wakati huu huonyesha kuwa kitendo kilikuwa kikiendelea wakati uliopita. likuwa na –ki– hutumika k.m. Juzi, mtoto alikuwa akicheza matopeni; Jana wanafunzi walikuwa wakisoma. Muhimu Ni makosa kutumia –likuwa pamoja na –na–. Mtoto alikuwa anacheza matopeni. X
- Wakati uliotimia (timilifu) hali ya kuendelea Huonyesha kitendo ambacho kimekamilika lakini kilikuwa kikiendelea muda mfupi tu uliopita. -likuwa na – m e – hutumika k.m. Mtoto alikuwa amecheza matopeni;
Wanafunzi walikuwa wamesoma.
- Wakati uliopita kufuatana kwa vitendo Hutuonyeshea kuwa, vitendo kadhaa vilifanyika kwa kufuatana. –li– hufuatwa na –ka– k.m. Badala ya: Aliamka. Alijitayarisha. Aliondoka. Alisafiri. Alifika. Tutasema: Aliamka, akajitayarisha, akaondoka akasafiri na akafika.
(Katika sentensi hii, tumetumia kiambishi –li– katika kiarifu cha kwanza kisha tukatumia –ka– katika viarifu vilivyofuata).
- Wakati ujao kutimia kwa kitendo Mtoto atakuwa amefika.