Insha za mwanzo

- Insha za sampuli hii huwa na sentensi ya kwanza ambapo mtahiniwa anatakikana kuendeleza sentensi hiyo. Katika insha ya aina hii, ni lazima mtahiniwa aisome sentensi ile ya mwanzo kwa makini na aelewe yanayotakikana kuandikwa. Lazima mtahiniwa aichambue sentensi aliyopewa kwa makini ili aelewe mkondo atakaoufuata katika kuandika insha yake.

Fikiria swali la aina hii:

Mnamo katikati ya kipindi cha pili, mwalimu wa zamu alizunguka madarasani huku akiwaeleza wanafunzi waende foleni …..                                                                                                                  

Ikiwa wewe ndiwe unayeiandika insha hii, lazima uyazingatie mambo kadhaa.

  • Si kawaida mwalimu kuzunguka madarasani na kuwaeleza wanafunzi waende foleni.
  • Si kawaida wanafunzi kwenda foleni mnamo kipindi cha pili na sanasana hata kufikia kiwango cha kukatiza curriculum. Bila shaka palikuwa na sababu kuu iliyofanya tukio hilo litendeke.

Kwa hivyo, katika uandishi wako, lazima uonyeshe ni tukio lipi hilo lisilokuwa la kawaida k.m. kutekwa nyara kwa mmoja wa wanafunzi pale shuleni; maafisa wa afya kuja kutoa chanjo za dharura za kukingia ugonjwa fulani hatari uliozuka n.k. Basi itambidi mwanafunzi mtahiniwa kuchagua mkondo fulani hatimaye aufuate katika uandishi wake wa insha. Mfano mwingine: Alfajiri moja nilipokuwa nikielekea shuleni, nilimsikia mtoto akilia katika vichaka vilivyokuwa kando ya barabara …………

 

Mambo ya kufikiria:  

Ni alfajiri: 

  • Mtoto anafanyaje vichakani wakati huo?
  • Yu pekee au ana mzazi?
  • Amefikaje vichakani?
  • Labda ametupwa na mama yake?
  • Labda alipotea njia na kulala pale kichakani?
  • Labda mama yake alishambuliwa na wezi na kuuawa au kujeruhiwa sana lakini mtoto akanusurika? Labda alitupwa pale na watekanyara?
  • Labda alitumiwa kama chambo na watekanyara ili ukienda kumwangalia ukamatwe.
  • Chagua mkondo utakaofuata kisha uuandike mtungo wako huku ukieleza yale uliyoyafanya na yaliyokupata k.m. ulifanyaje baada ya kusikia kilio kile cha mtoto?
  • Ulienda kutazama au ulikimbia kuwajulisha watu?
  • Yapi yaliyofuata?
  • Eleza hisia zako k.m. uliogopa/ukawa na wasiwasi/mshtuko, n.k.

 

Zoezi

Andika insha ukianza na haya uliyopewa:

1. Safari yetu ilianza salama salimini. Hata hivyo tulipofika …

2. Simu ilipolia, niliinyanyua na nilipoongea, niliitambua sauti ya ndugu yangu aliyekuwa huko ng’ambo …

3. Mvua ilipoendelea kunyesha kupita kiasi pale kijijini …

4. Kipenga kilipolia, wachezaji wa timu zote mbili walijitosa uwanjani …

5. Jioni hiyo, mzazi wangu alirejea nyumbani akiwa na huzuni …

6. Mnamo usiku wa manane, nilisikia jirani yangu akipiga kamsa …

7. Nilimsubiri ndugu yangu pale kituoni mwa mabasi lakini hakufika. Hiyo ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kufika mjini. Giza lilipoanza kutanda …

8. Mnamo usiku huo, mvua ilizidi kunyesha. Nilikuwa nimebaki sebuleni nikiyadurusu curriculum yangu. Mara nilisikia mtu akibisha mlango huku akiitana kwa sauti nyonge …

9. Tulikuwa tukisikiliza taarifa ya habari redioni. Mara jina langu likatajwa kuwa mwanafunzi bora katika mtihani wa kitaifa kote nchini …

10.Nilipoiangalia nambari ile tena niligundua kuwa nilikuwa mshindi wa shilingi milioni moja pesa taslimu …