Makosa yafanywayo
- Kutosoma insha mara tu baada ya kuiandika. Ni vizuri kusoma insha ili kuyasahihisha makosa uliyoyafanya wakati wa kuandika.
- Kutumia maneno usiyokuwa na uhakika kuyahusu. Badala yake, unafaa kuuliza au kufanya utafiti kuyahusu maneno yale.
- Kukatakata maneno k.m angesoma nilipo fika badala ya nilipofika. aliye kuita badala ya aliyekuita. ku sherehekea badala ya kusherehekea.
- Kuyashikanisha maneno k.m. Kwasababu badala ya kwa sababu Kwanini badala ya kwa nini Yakwamba badala ya ya kwamba Ilinifike badala ya ili nifike
- Maendelezo mabaya k.m. inchi badala ya nchi, kuwa badala ya kua, kusheherekea badala ya kusherehekea, tama badala ya tamaa, alafu badala ya halafu, ilibidii badala ya ilibidi.
Mwanafunzi anashauriwa kuepuka baadhi ya maneno hayo na kutumia visawe vyake
k.m. hatimaye/baadaye badala ya halafu, taifa badala ya nchi n.k.
Aidha, anashauriwa kuvisoma vitabu vingi vinavyofaa ili kuondolea mbali udhaifu huu. Ikumbukwe kuona si sawa na kusikia. Aidha:
- Kutumia sentensi ndefu na za kuchosha. Mwanafunzi anashauriwa kutumia sentensi fupi na sahihi. k.m. Alfajiri hiyo nilikula staftahi yangu. Nilichukua mkoba wangu wa vitabu. Niling’oa nanga kuelekea shuleni. Nilifika shuleni salama salmini n.k.
- Kuegemea mambo kama vile siasa, dini, ukabila, jinsia n.k. k.m. Ni makosa katika insha yake mwanafunzi kujaribu kud•haralisha jinsia fulani, kabila fulani, dini au dhehebu fulani.
- Matumizi ya maneno yasiyo ya Kiswahili. Sharti ieleweke kuwa, matu•mizi ya neno lolote lisilo la Kiswahili yatabeba adhabu kali katika kutuza alama. Haijalishi hata maneno hayo yakiwekwa alama za kunukuu.
- Matumizi ya maneno ya mkato kama vile mamake, babaye yaepukwe.
- Maneno ya kishairi kama vile banati, abu, bati n.k. yaepukwe kabisa.
Wakati wa kusahihisha insha za mtihani, alama hutuzwa kulingana na vile ambavyo mwandishi ameshughulikia kila kipengele miongoni mwa vipengele vitano vifuatavyo:
- Maudhui
- Msamiati na muundo
- Mpango na mtindo
- Mtiririko na mshikamano
- Sarufi na maendelezo (tahajia)
Kila kipengele huwa kimetengewa alama fulani. Mtahini anastahili kutuza alama kwenye kila kipengele kisha kuzijumlisha kwa usahihi ili kupata alama jumla. Basi ni vyema sana kila mwanafunzi aelewe vipengele hivyo ni vipi na mahitaji ya kila kipengele. Hilo litamwezesha kujiandaa vilivyo.